SEX MACHINE - SEHEMU YA 04
SEHEMU YA 04
Hivi mnajua hii kazi ni ya kuchambua mchicha eenh! Inabidi muwe ngangari kwenye kampuni hii na sitawavumilia watu wazembe tena. Mtakufa." Ikamaliza sauti hiyo kwa kutoa kalipio baya sana kwa washirika wote wa humo ndani kisha mkoromo wa spika ukafuatia na kufuatiwa na ukimya kuashiria kuwa mkuu huyo alishakata mawasiliano. Minong'ono midogo midogo ikaibuka mahali hapo huku vijana maalumu wakihangaika na kuutoa mwili wa Mahmood eneo hilo. Joesan na Suzane wakaondoka na kuwaacha watu hao wakizidi kung'atana masikio na jambo likijadiliwa hapo ni namna Joesan atakavyoweza kumpata Sex Machine kwa muda huo mfupi ambao Suzane aliahidi. Kwao waliona ni jambo lisilowezekana na ni kama walijivalisha njuga na ilhali kucheza ngoma lilikuwa ni timbwili kubwa.
"Kwanini huyu binti anajipendekeza sana kwa Joesan?" aliuliza mzee mmoja wakiwa wawili baada ya kutoka kwenye ule ukumbi wa mikutano.
"Mgobo, Suzane ni lazima ampigie kifua Joesan, kwani yule ni bosi wake na anafanya kazi chini yake tukiachilia mbali ukaribu walionao." Akazungumza mzee wa pili.
"Naona kama anajipalia makaa mwenyewe, Mkuu si mtu mzuri kabisa ujue?"
"Haijalishi Mgobo na hiyo ni juu yao tunachotakiwa sisi ni kuomba hiyo mashine ya ngono ipatikane bila hivyo ajira zetu zipo mashakani maana kampuni yetu ipo katika hatua mbaya sana, sasa hii ni hatari mno."
"Haya ndiyo matatizo ya kuongozwa na kijana mdogo mzee mwenzangu, lazima aende kinyume tu." Walizidi kunong'ona wazee hao kisha kila mmoja akapita njia yake na kuelekea kunako mhusu. Joesan baada ya kuingia ofisini kwake akiwa na Suzane, alijitupa kitini mwake na mwanadada huyo naye akajitwalia nafasi yake akaketi. Joesan akafikiri kwa muda kisha akavuta pumzi nyingi ndani ya mapafu yake na kuziachia kwa mkupuo, akasema;
"Umefanya nini sasa Suzane, kile ulichokisema pale kumbe ndicho ulichokuwa umekipanga?"
"Ulitaka nisemeje Bosi, tulikuwa hatuna utetezi mwingine pale na niliona kuwa hukuwa na njia nyingine ya kiweza kumshawishi mkuu hadi aweze kukuelewa na nilikuwa na hofu sana maana huwenda kosa lako likaweza kutuletea madhara sisi wote. Unafikiri ningetoa wazo gani ambalo Mkuu angeliafiki? Wewe mwenyewe nadhani umeona kilichomtokea yule mwarabu. Hakukuwa na cha kujibu Bosi zaidi ya kile na sidhani kama kuna sababu ya kulaumiana kwenye hili." Alisema Suzane. Pamoja na maneno yale aliyoyasema Suzane hata hivyo Joesan alipingana na maneno ya mwanadada huyo hakumuelewa hata kidogo. Kitendo kile cha Suzane kutoa oda kuwa Sex Machine atapatikana ndani ya siku tatu, hilo lilikuwa ni jambo gumu kabisa na alishindwa kuelewa mategemeo mazima ya mwanadada huyo yalikuwa ni yepi.
"Pamoja na hayo hata hivyo si kwa jibu lile, pale tumeshajitia kitanzi wenyewe Suzane... Ok, haya tunafanyaje sasa maana hata sielewi." Akalalamika Joesan. Alichanganyikiwa haswa na hakuelewa namna atakavyofanya kuhusiana na maamuzi yale yaliyotolewa na mkuu.
"Sikiliza Joesan," alizungumza binti huyo na kumtazama bosi wake usoni, akaendelea.
"...kwa sasa hauko sawa Boss hata kama tutaongea, hatutafikia muafaka mzuri, chakufanya mimi nitakuja nyumbani kwako jioni na ni lazima hili tulipatie ufumbuzi kabla ya siku ya kesho. Tutaongea kwa utulivu mkubwa nitakapofika nyumbani kwako."
"Kabla ya kesho...yaani unamaanisha kabla ya kesho ufumbuzi uwe umepatikana...?" Joesan akahoji kwa mshangao.
"Ndiyo, ukumbuke ni kama tumesaliwa na siku mbili pekee?"
"Najua lakini nashangaa wewe kusema kabla ya kesho tuwe tumepata ufumbuzi wa hili. Unajua unanichanganya sana Suzane, kwani unampango gani wewe mwanamke?" Akahoji tena Joesan bado alikuwa katika mkanganyiko mkubwa wa mambo na hakumuelewa huyo binti kabisa.
"Acha papara Bosi najua nini tutafanya," akajibu. Joesan aliurudisha mgongo wake nyuma ya kiti na kuegamia. Akapiga kite cha hasira na uchovu kisha akavuta faili fulani pale mezani akachukua na kalamu na kukaa katika mkao wa kutaka kuandika jambo lakini hakuandika chochote, akaishia kuizunguusha ile kalamu vidoleni mwake na kuirudisha kwenye kopo maalumu lililojaa kalamu za rangi mbalimbali akalifunga lile faili. akatafakari hili na lile kwa haraka haraka mara mlio wa simu ukamshtua. akaipokea na kuiweka sikioni baada ya kulitambua jina la mpigaji.
"Nimemaliza mihangaiko sasa nafikiri leo ni nafasi nzuri ya mimi na wewe kukutana, nipo Morogoro Hoteli." Ilisema sauti hiyo kutoka upande wa pili wa simu hiyo.
"Ok, kaka nakuwa hapo sasa hivi" akaikata na kuitia kwenye mfuko wa koti lake na kusimama. alilinyakuwa faili fulani akalifukia kwenye mtoto wa meza kisha akamgeukia Suzane.
"Naomba umalize kila kitu kinachonihusu mimi kikazi, ikiwa kuna mtu atanihitaji utamwambia anitafute kwenye namba yangu binafsi. Natoka kidogo na sitarudi tena, tutaonana jioni mimi na wewe," Suzane akajibu sawa. bwana huyo akatoka hadi ilipo Toyota prado nyeusi, akapakia garini humo na kuondoka. Alifika Morogoro Hoteli akapitiliza ndani kabisa ya Hoteli hiyo kubwa mjini hapo ikiwa tu ni mara baada ya kupata maelekezo ya mwenyeji wake mahali alipo alipofika idara ya mapokezi. Alifika hadi mahali alipoelekezwa na kumkuta mwenyeji wake akiwa katulia kitini akipata kinywaji ghali kabisa. Mbele yake kukiwa na kiti kimoja ambacho ndicho alichokitwaa Joesan akaketi.
"Habari za masiku tele bwana Babu Ally?" Ndivyo walivyoanza maongezi yao namna hiyo.
"Nzuri tu ndugu yangu, ni siku nyingi kweli maana ni muda mrefu hatujaonana. vipi yule kijana wako ni mkubwa sana sasa hivi?"
"Aah! Unamzungumzia Chriss?"
"Haswaa huyohuyo,"
"Ni mkubwa sasa hata masomo amemaliza, yupo nyumbani kwa sasa," alisema Joesan.
"Ndiyo, vipi 'wife' naye anaendeleaje?" Aliuliza Babu Ally na Joesan akajibu.
"My wife keeps well na ni wa afya tele kabisa shida hakuna." Wakati wakiwa wanaendelea na salamu za kawaida, muhudumu akafika mahali hapo na kuchukua oda na kuondoka akiwaacha mabwana hao wakiendelea kupepeta domo.
"Nimetoka ughaibuni juzi na huu ni mguu wako bwana Joesan maana huu ndiyo ule muda tulioupanga wa mimi na wewe kukutana. Unajua ni muda sasa tangu biashara yetu isimame, naona tuna kila sababu sasa ya kuirudisha tena au unasemaje Joesan?" Akaacha swali Babu Ally. Wakati Joesan akiwa anafikiria kulijibu akaongeza.
"Hatukuwa na mawasiliano mazuri hapa katikati kiasi kwamba hatukuweza kuzungumzia mustakabali mzima wa biashara zetu. Tutazifanya kwa namna gani Joesan nadhani unajua kuwa utajiri wetu unategemea hizi biashara kwa asilimia kubwa?"
"Babu Ally kakaa, najua sana hilo na hivi unavyoniona siko sawa ndugu yangu. Huko ofisini ni moto," akanyamaza kidogo, akameza mate na kuendelea.
"Mkuu amenijia juu vibaya sana. Si unajua yule Sex Machine alikufa katika harakati za kuupigania mzigo wetu huko Australia?" Aliuliza Joesan.
"Ndiyo," Babu Ally akajibu.
"Sasa nimepewa siku tatu tu za kumrejesha Sex Machine ndani ya kampuni."
"Come on Joesan! Wewe...?" Alishtuka Babu Ally baada ya kuambiwa jambo lile na kusema.
"Sasa wewe utampatia wapi huyo Sex Machine ndugu yangu lakini kwanini ameamua kukufanyia hivyo sasa?"
"Hapa ninapozungumza haya hata sielewi ndugu yangu lakini Mkuu hana kosa kwa hili, kwasababu hata yeye anachong'ang'ania ni kwamba Sex Machine alikufa nje ya kazi za kampuni naa...!"
"Hebu ngoja kidogo, muhudumu analeta chakula," Babu Ally akamkatisha na kuifanya sentensi yake kuelea hewani. Chakula kikawekwa mezani kila mmoja akijiweka mkao wa kula huku wakiendelea na maongezi yao.
"Na isingekuwa urafiki wetu kati yangu na Mkuu...!"
"Wee! Angekwisha kukuuwa zamani aisee." Alidakia Babu Ally.
"Sasa tunafanyaje maana tunataka kuifanya hii biashara kitaalamu zaidi. Nimetafuta watu wa kuwatumia lakini sioni kama watafiti kwemye hili." Aliongeza Babu Ally.
"Achana na hao watu kwanza na naomba huu mjadala tuufunge, acha mimi nikatafakari kwa kina nyumbani kesho nitakuwa na jibu zuri la kukupa. Kwasasa ni uwongo nimechanganyikiwa sana acha niende nyumbani nikapumzike." Alizungumza Joesan.
"Vipi chakula naona umegusa tu kaka?"
"Utanisamehe kaka sioni kama hicho chakula kina ladha yoyote wacha niende nyumbani nikajipe muda mwingi wa kufikiria na nijue nini cha kufanya." Akasema akaondoka. Babu Ally alitikisa kichwa kwa masikitiko makubwa. Alimhurumia sana jamaa yake huyo lakini hakuwa na jinsi ya kufanya na aliogopa sana kujihusisha na hilo jambo japo kwa namna moja au nyingine, upotevu wa Sex Machine unamhusu na wote walishiriki lakini hakutaka kabisa kulisogelea jambo hilo karibu. Shughuli ya huyo mtu anayejiita mkuu alijua vilivyo.
"U.tanisamehe Joesan kwa hili, bado napenda kuishi." Ndivyo alivyokuwa akiwaza Babu Ally. Joesan alitoka hadi nje ya ile hoteli na kujiingiza garini mwake, alifunga mlango wa gari vizuri pamoja na kuufunga mkanda kisha akajilaza kwenye kiti hicho cha dereva akiweka hili na kupangua lile kabla ya kulirudisha hili. Baada ya muda kidogo alinyanyuka na kuwasha gari yake hiyo, ila kabla ya kuliondoa, aliwasha redio na kuutafuta wimbo wa mwanamama Celine Dion. wimbo unaokwenda kwa jina la 'That the way It is'. ambao aliamini kidogo unaweza kuyapeperusha mawazo yake kwa muda huo.
Comments
Post a Comment